Siku ya kuzaliwa: Odemba aungana watoto wenye uhitaji
- Charlii Media
- Feb 13
- 2 min read

Mwanamitindo wa kimataifa, Miriam Odemba, anatarajiwa kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa kwa kusherehekea pamoja na watoto wenye ulemavu katika shule ya Msingi ya Jeshi la Wokovu jijini Dar es Salaam.
Hafla hiyo fupi inaakisi dhamira yake ya muda mrefu katika kuendeleza upendo, ujumuishaji wa jamii, na huduma kwa makundi maalum.
Akizungumza kuhusu tukio hilo, Mwalimu Ibra wa shule hiyo amesema kuwa uhusiano wa Miriam na watoto hao umekuwa thabiti na utamaduni wa kila mwaka.
“Upendo wa Miriam kwa watoto hawa hauna kipimo,” alisema. “Uwepo wake huwaletea furaha kubwa, na kwa sasa washaanza kujiandaa kwa hamasa kubwa.”
Kwa mujibu wa uongozi wa shule, Miriam amekuwa akifanya kuwa desturi ya kuwatembelea watoto hao kila anapokuwepo nchini Tanzania, akigeuza kila ziara kuwa tukio la furaha na mshikamano.
Watoto, wamekuwa wakimchukulia kama dada mlezi, na wamepanga kumuandalia burudani mbalimbali, ikiwemo ngoma za asili na onesho maalum la mitindo kupitia klabu yao ya mitindo.

Shule hiyo imekuwa ikihudumia watoto wenye ulemavu kwa miaka mingi chini ya uangalizi wa kanisa la Jeshi la Wokovu, huku ikifanya vizuri kitaaluma na kuhamasisha michezo, sanaa, na burudani kama sehemu ya maendeleo kwa wanafunzi.
Miriam pia amekuwa chachu ya kuanzishwa kwa kikundi cha mitindo shuleni hapo, ambacho tayari kimeshiriki katika maonesho mbalimbali, ikiwemo ya Kawe mwaka jana na katika ufunguzi wa Sauti ya Mitindo 2025.
Kwa upande wake, Miriam amesema kusherehekea siku yake ya kuzaliwa na watoto wenye ulemavu ni jambo la maana sana kwake, na humletea amani na furaha ya kweli.

“Ninawapenda watu wote, na natamani jamii yangu ifahamu kuwa watu wa makundi maalum nao wanapenda kufurahi, furaha yao ni halisi na safi,” alisema katika mahojiano maalum.
Kupitia Taasisi ya Miriam Odemba Foundation, Miriam amekuwa akitoa misaada kwa zaidi ya miaka saba sasa, akisaidia wajane, watoto, watu wenye ulemavu, na mabinti wanaosoma, akisisitiza ushawishi wa kweli kwa huduma kwa jamii.


Comments