top of page

Miriam Odemba Foundation Yadhamini Mchezo wa Kirafiki wa Waandishi wa Habari, Yatoa Wito wa Umoja Kupitia Michezo

  • Writer: Charlii Media
    Charlii Media
  • Jul 12
  • 2 min read

Na Charles Mkoka

Katika kuhamasisha mshikamano na afya kwa vijana, Taasisi ya Miriam Odemba Foundation (MOF) imedhamini rasmi mchezo wa kirafiki wa mpira wa miguu kati ya waandishi wa habari wa JUMIKITA na timu ya Middo Store, uliochezwa katika viwanja vya GSM, Mikocheni B jijini Dar es Salaam.


Raykhan, a representative of the Miriam Odemba Foundation, addresses the press following the match between Journalists and Middo Store in Dar Es Salaam
Raykhan, a representative of the Miriam Odemba Foundation, addresses the press following the match between Journalists and Middo Store in Dar Es Salaam

Akizungumza kwa niaba ya taasisi hiyo, Raykhan – ambaye ni mwakilishi wa MOF – amesema mchezo huo ni sehemu ya mikakati ya taasisi hiyo katika kuimarisha uhusiano kati ya vijana, waandishi wa habari na taasisi mbalimbali, huku pia ukilenga kujenga mshikamano na kukuza maadili chanya kupitia michezo.

“Sisi kama taasisi tumejipanga kujenga mahusiano mazuri na kila kundi ndani ya jamii. Tunatambua nafasi ya michezo katika kuunganisha watu na kuhamasisha maadili ya mshikamano, umoja na afya ya akili kwa vijana,” amesema Raykhan.

Katika mchezo huo uliojaa ushindani wa kirafiki, timu ya Middo Store iliibuka na ushindi wa mabao manne kwa mawili dhidi ya JUMIKITA. Nahodha wa Middo Store, Rimaly Odemba – ambaye pia ni mmoja wa waasisi wa kampeni hiyo – amesema matokeo hayo ni kielelezo cha namna michezo inaweza kuwa jukwaa la kuleta furaha na mshikamano, kuliko ushindani wa kawaida.

“Tulicheza kwa upendo. Huu ni ushindani wa kirafiki, na furaha imeonekana. Tunapongeza timu zote kwa kujitokeza, na tunatarajia kuendelea na matukio kama haya zaidi,” amesema Rimaly.

Kwa upande wa JUMIKITA, beki wa timu hiyo, Noveth Mhagama, amesema michezo kama hiyo ina nafasi kubwa ya kuwasaidia vijana kuepuka makundi hatarishi na badala yake kujenga mtandao wa ushirikiano mzuri kati ya wanahabari na jamii.

“Tumeona jinsi ambavyo mchezo umeamsha morali. Hii ni njia mojawapo ya kuwaweka vijana mbali na vishawishi vya uhalifu na badala yake kuwahamasisha kushirikiana na taasisi mbalimbali,” alisema Mhagama.

Tukio hilo pia lilihusisha kauli za shukrani kutoka kwa baadhi ya washiriki wa mchezo huo. Mawinza, ambaye alikuwa nahodha wa JUMIKITA, amesema:

“Huu ulikuwa mchezo wa kuonesha kwamba michezo inaleta furaha. Sio suala la nani alishinda bali kuonesha mshikamano wa pamoja.”

Mchezo huo umetajwa kuwa sehemu ya hamasa inayoenda sambamba na kampeni inayokuja ya kutembelea wajawazito na wanawake waliojifungua, inayotarajiwa kufanyika Julai 25, 2025. Kampeni hiyo imebuniwa na kufadhiliwa na mwanamitindo wa kimataifa mwenye makazi yake Paris, Miriam Odemba, kupitia taasisi yake ya MOF.

 
 
 

Comments


bottom of page